Wednesday, June 13, 2012

ARSENAL WAKOMARIA UEFA


Manchester England
“NAONDOKA Arsenal kwenda Manchester City, siyo kwamba naichukia Arsenal, hapana, naipenda sana lakini nakwenda City kufuata makombe.”
Hiyo ni kauli ya kiungo wa Manchester City, Samir Nasri wakati anaondoka kwenye kikosi cha Arsenal na kujiunga na City.
Mshambuliaji huyo jana ndiyo alikuwa chachu ya Manchester City kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya QPR na kumaliza ukame wa miaka 44 bila kutwaa ubingwa wa England.
Wakati City ikipata bao la tatu, mechi kati ya Manchester United ilikuwa imeshamalizika kwa United kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sunderland, shukrani kwa bao safi lililofungwa na Wayne Rooney.
Lakini haikuwa hivyo, burudani ya kutosha ilikuwa kwenye Uwanja wa Etihad ambao mpaka dakika ya tisini ya mchezo, City ilikuwa nyuma kwa mabao 2-1.
Pablo Zabaleta aliifungia Man City bao la kwanza katika dakika ya 39, Djibril Cisse aliisawazishia timu yake katika dakika ya 48, Jamie Mackie akatupia la pili katika dakika ya 66.
Kiungo wa QPR, Joel Barton, alipewa kadi nyekundu baada ya kumpiga kiwiko, Carlos Tevez na kuanzia hapo QPR walilinda lango lao kwa asilimia 90, hali iliyowafanya wawe majaribuni mara kwa mara.
Pamoja na City kushambulia kwa nguvu zote, iliwabidi kusubiri hadi dakika ya tisini ili kupata bao la kusawazisha lililowekwa kimiani na Edin Dzeko lakini ziliongezwa dakika tano na katika dakika ya nne, Sergio Aguero akaifungia timu yake bao la tatu na la ushindi.
Nafasi ya tatu
Arsenal ilipambana na kufanikiwa kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye mchezo mgumu dhidi ya West Bromwich.
Arsenal ilianza kufunga kupitia kwa Yossi Benayoun, Bromwich wakasawazisha kupitia kwa Shane Long katika dakika ya 11, Graeme Dorrans aliifungia timu yake bao la pili katika dakika ya 15.
Lakini Arsenal ilicharuka na kupata mabao mawili kupitia kwa mabeki André Santos katika dakika ya 30 na Laurent Koscielny dakika ya 55.
Tottenham Hortspur, ilimaliza katika nafasi ya nne baada ya kushinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Fulham, shukrani kwa mabao yaliyofungwa na Emmanuel Adebayor na Jermaine Defoe.
Newcastle imemaliza katika nafasi ya tano baada ya kukubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Everton.
Zilizoshuka
Bolton, Blackburn na Wolves zimeshuka daraja, Bolton ilikubali sare ya mabao 2-2 dhidi ya Stoke City na kuungana na Blackburn na Wolves ambazo zilishashuka.
Matokeo mengine
Chelsea iliichapa Blackburn mabao 2-1, Norwich ikaichapa Aston Villa 2-1, Swansea ikaichapa Liverpool 1-0, Wigan ikaichapa Wolves mabao 3-2.

No comments:

Post a Comment