Friday, July 13, 2012

One. Uno. Moja. Eins. Een. 한. Une. Jeden. En. Yksi. 1. I. один…
Wengine itabidi wachague kuanzia mbili mpaka tisa!
One The Incredible.
Ni mmoja wa wasanii wa Hip Hop ambao wanaangaliwa kwa jicho la tatu. Nimepata nafasi ya kusikiliza nyimbo zake zote, ambazo bila shaka zinawapa matumaini mashabiki wa Hip Hop Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla kuwa gemu inaanza kuimarika.
Sasa hivi kuna fukuto na msisimuko wa Hip Hop mitaani, na One ni mmoja ya ‘madogo’ ambao wamelianzisha. Nina uhakika ameshajipatia Stans wa kutosha mpaka sasa hivi ingawa anadai kuwa safari yake bado ni ndefu.
Wakati mixtape ya Music Lab The Element — iliyosukwa na Duke Tachez akishirikiana na One, Stereo na Nikki Mbishi — ikiendelea kugombaniwa mitaani, tumeona ni vema kumtafuta One na kufanya mahojiano mafupi.*
1.Tunafahamu kuwa uko mwaka wa kwanza sasa hivi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwanini umeamua kuingia kwenye Hip Hop? Kuna mtu aliyekusukuma au kukwambia kuwa una kipaji cha kuandika mashairi na kughani?
Kwa kweli sio kwamba naingia kwenye Hip Hop, mimi nipo kwenye hii ‘game’ kwa muda mrefu tu.  Nilianza kujihusisha na muziki huu wa ‘kuchana’ (kughani) tangu nikiwa nina miaka sita. Enzi hizo ma-MC — kama kina SOS B — walikuwa wanakuja nyumbani kwetu kwa ajili ya rehearsals (mazoezi). Kwasababu kipindi hicho kaka zangu nao walikuwa kwenye zile harakati za muziki wa Hip Hop; pamoja na kina Zavara na wasanii wengine kwenye miaka ya 1994, 95, 96 na kuendelea…
Tokea enzi hizo mi’ ndio nilipoanza safari yangu ya Hip Hop.  Na nikajikuta kila siku kiwango kinaongezeka siku baada ya siku! Pia watu kama Prof. Jay, Fid Q na Hashim “Dogo” wamenishawishi (influence) kwa kiasi kikubwa.
2. Wewe na wenzako mnachukuliwa kama “kizazi kipya” cha Hip Hop Tanzania? Nini matarajio na malengo yenu kwenye Hip Hop kama damu changa kwenye game?
Ninashukuru kufahamu kwamba na mimi ni mmoja kati ya MC’s wanaochukuliwa kuwa na uwezo, ingawa ndoto yangu haikuwahi kuwa hivyo. Mi’ napenda Rap Music, lakini siwezi kuongelea mipango yangu sasa hivi  kwasababu bado (ni) mapema sana.
Kwa upande mwingine najaribu kutilia mkazo shule zaidi. Muziki ni kitu ambacho nimekua nacho, na kwa mtazamo wangu nadhani kipaji changu kimekuwa kikiongezeka kutokana na ukuaji wangu wa upeo na maarifa. Kwa hiyo, kama nikiendelea kuhakikisha nipo sambamba na ujuzi na maarifa, basi nitaendelea kuwa sambamba na Hip Hop!
Ni matumaini yetu ipo siku tutaweza kuipeleka ‘game’ nje ya mipaka (ya Tanzania)!
3. Mtazamo wako kwenye fani hii ukoje? Ni tofauti gani kati yenu nyie wa “kizazi kipya” kwenye na kile cha zamani?
Binafsi ninataka kufanya ‘game’ na kuipeleka nje ya mipaka ya Tanzania (international scale).  Mpaka sasa hivi ninatengeneza album na mixtapes zaidi, kwasababu tunataka kuufikisha muziki wetu mbali kadri tunavyoweza!
Ukuaji wa teknolojia nao utatusaidia; vitu kama blogs havikuwepo zamani , ila sasa hivi vinatusaidia kufikisha kazi zetu mbali zaidi ukilinganisha na kipindi kile. Hivyo tunajaribu kutumia zana hizi kujitangaza…
Adam, Suma, One, Prof. Jay, Nikki Mbishi, Stereo.
4. Nimesikiliza mashairi yako, na kusema ukweli una “flow” kali. Mashairi yamesimama; ingawa sio rahisi kuyaelewa haraka-haraka. Sasa, uandishi wako wa mashairi wa namna hii ni kitu ambacho hutokea tu au unafanya makusudi? Nini hukupelekea wewe kuandika unachoandika na kuwasilisha jinsi unavyowasilisha kazi yako.

Hip Hop ni utamaduni, na uwasilishwaji wake, ambao ni kupitia rap, ni sanaa.
Lakini wakati huo huo ni maoni au mtazamo binafsi (wa fanani) kuhusu mambo yanayomzunguka.  Hivyo mimi ninawasilisha kile ambacho ninachokiona kila siku kwenye jamii kadri ya upeo wa maarifa na ujuzi wangu.
Kawaida uwasilishaji wa aina yoyote unatokana na wasifu/tabia ya mtu anayewasilisha, au uelewa wake juu ya kile anachokijua. Kwa kifupi, utunzi wangu unatokana na vile ninavyoelewa ninayoyasema, na vile vile (jinsi) ninavyotaka nieleweke!
5. Ulitoka na ‘One The Incredible’, ambayo imepokelewa vizuri sana. Kisha ‘Pure Namba’, ambayo nayo ni kali (kwa mtazamo wangu ‘Pure Namba’ ni kali zaidi!). Ila sidhani kama imepokelewa na ma-DJ kama ile ya awali. Unalichukuliaje hili? Wewe binafsi unadhani ipi ni nzuri zaidi?
Ulichokisema kuhusu ‘Pure Namba’ ni kweli, ila mwisho wa siku inaishia kwa wasikilizaji. Yaani, hata kama wimbo ukibaniwa, mara nyingi mashabiki wanazipata hizi ngoma kwasababu wanazitafuta wenyewe.
Ila sijawahi kukutana na mtu ambaye hana ngoma ya ‘Pure Namba’…  na nime’shakutana na watu ambao hawana ‘Incredible’!
Mi’ binafsi naikubali ‘Incredible’!
Nimefurahishwa na jinsi One anavyojaribu kufikiria njia za kuipeleka kazi yake nje ya Tanzania. Je, unadhani wahusika (Music Lab) wanatumia njia sahihi? Au unadhani kuna sehemu ambazo wanapaswa kufanya marekebisho?
Tunapenda kuchukua nafasi hii kumtakia kila la heri One na wasanii wenzake wenye malengo kama yake. Inawezekana…
Moko!… Mi’ binafsi bado naikubali ‘Pure Namba’. Zaidi!

No comments:

Post a Comment